JIANDAE KWANZA KUPOKEA JIBU KABLA HUJAULIZA SWALI

Mama mmoja alikwenda Mahakamani kutoa ushaidi dhidi ya mshitakiwa aliyeiba kandambili msikitini. Ulipofika muda wa yeye kuulizwa maswali na wakili anayemtetea mshitakiwa, wakili alinyanyuka kwa mbwembwe huku akielekea kwenye kizimba alichokuwa yule mama. Basi kwa kujiamini kabisa yule wakili akaanza na swali hili: “Je, unanifahamu mimi ni nani?” basi yule mama akajibu “ nakufahamu vizuri sana, ulikulia mtaani kwetu na kipindi ulipokuwa mdogo ulikuwa na tabia njema sana ila sasa umebadilika na umekuwa na kiburi, jeuri na dharau sana, mbaya zaidi umekuwa na tabia ya kutembea na wake za watu.”

Wakili kwa kuchanganyikiwa na jibu alilopewa basi akamwelekezea kidole Jaji huku akimuuliza yule mama “Je unamfahamu yule ni nani?” Mama kama kawaida akaanza kutoa maelezo yake hivi: “Huyo hapo pia namfahamu vizuri kwani mlikuwa naye pamoja nashangaa kwa nini unaniuliza kama namjua, hata yeye kama ulivyokuwa wewe alikuwa kijana mtiifu sana lakini tangu alipoajiriwa amekuwa na tabia chafu kama zako na pia ile tabia yake ya kutembea na wake za watu juzi tu alimdanganya mkewe kuwa anakwenda safari kikazi kumbe alikwenda kulala na mwanamke Gesti na mbaya zaidi alilala na mkeo wakati anajua fika kuwa yule ni mke wa rafiki yake mkubwa.

Jaji akiwa ameishiwa pumzi kabisa akasimama na kusema: “Sikilizeni nyie Nguchiro, yeyote atakayemuuliza huyu mwanamke swali lolote kuhusu mimi basi atakwenda yeye Gerezani badala ya mshitakiwa.”

No comments: